Home Habari Kuu Watu wanne wafariki katika ajali Nakuru

Watu wanne wafariki katika ajali Nakuru

0

Watu wapatao wanne wamefariki kwenye ajali ya leo alfajiri katika eneo la Salgaa kwenye barabara kuu ya kutoka Eldoret kuelekea Nakuru.

Kulingana na maafisa wa polisi, abiria wengine wanane walipelekwa hospitalini baada ya kupata majeraha kwenye ajali hiyo iliyotokea saa tisa alfajiri leo.

Ajali hiyo ilihusisha gari la kubebea abiria aina ya Toyota Hiace ya kampuni ya Eldoret Crossroads Shuttle ambayo ilikuwa inatoka Eldoret kuelekea Nakuru na Trela.

Gari hilo la abiria linasemekana kugonga trela iliyokuwa imeegeshwa barabarani na ambayo ilitoweka punde baada ya ajali.

Wanawake watatu na mwanaume mmoja walithibitishwa kufariki papo hapo na miili yao ikapelekwa kwenye hifadhi ya maiti ya kaunti ya Nakuru ambapo inasubiri uchunguzi na utambuzi.

Gari hilo lilibururwa hadi kituo cha polisi cha Salgaa kwa uchunguzi zaidi huku polisi wakianzisha msako dhidi ya trela iliyohusika kwenye ajali hiyo.

Shirika la uchukuzi na usalama barabarani NTSA lilitoa takwimu kuhusu ajali za barabarani ambazo zilibainisha kwamba wanaotembwa kwa miguu ndio wameathirika zaidi kwenye ajali kati ya Januari Mosi na Aprili Mosi mwaka 2024 ambapo 436 walifariki.

Katika kipindi sawia mwaka jana, idadi hiyo ilikuwa watu 374. Waendesha pikipiki waliofariki kwenye ajali kwenye robo ya kwanza ya mwaka 2024 ni 276 ikilinganishwa na 311 waliofariki katika kipindi sawia mwaka jana.

Website | + posts