Home Habari Kuu Watu sita wafariki katika ajali ya barabarani Narok

Watu sita wafariki katika ajali ya barabarani Narok

Kulingana na maafisa wa polisi, dereva wa gari aina ya Subaru aligongana ana kwa ana na gari aina ya Toyota Sienta iliyokuwa ikitoka upande wa pili, iliyokuwa na abiria sita.

0
Watu sita wafariki katika ajali ya barabarani kaunti ya Narok.

Watu sita wamefariki na wengine saba kujeruhiwa, kufuatia ajali ya barabarani katika kaunti ya Narok.

Ajali hiyo iliyohusisha magari mawili, ilitokea karibu na eneo la Silanka, kwenye barabara ya Narok-Mulot, kilomita nne kutoka mji wa Narok.

Kulingana na maafisa wa polisi, dereva wa gari aina ya Subaru aligongana ana kwa ana na gari aina ya Toyota Sienta iliyokuwa ikitoka upande wa pili, iliyokuwa na abiria sita.

“.. gari aina ya Toyota Sienta, ilikuwa ikielekea upande wa Mulot, huku gari aina ya Subaru ilikuwa ikielekea upande wa Narok. Magari hayo mawili yaligongana ana kwa ana wakati Subaru ilipokuwa ikijaribu kupita gari lingine,” ilisema taarifa ya polisi.

“Kufuatia ajali hiyo, dereva wa gari aina ya Sienta na abiria wengine watano walifariki papo hapo,” iliongeza taarifa hiyo.

Aidha dereva wa gari aina ya Subaru alipata majeraha ya kifua na kupelekwa katika hospitali moja katika eneo hilo kwa matibabu.

Magari hayo mawili yalipelekwa katika kituo cha polisi cha Narok.