Takribani watu 70 wakiwemo watoto wameuawa baada ya genge moja kuvamia mji mdogo nchini Haiti.
Aidha watu 16 walijeruhiwa vibaya kulingana na habari za umoja wa mataifa, kuhusu shambulizi la kundi hilo linalojulikana kama Gran Grif katika eneo la kati mwa taifa hilo.
Magenge yaliyojihami yamechukua udhibiti wa maeneo kadhaa nchini Haiti.
Kikosi cha maofisa wa polisi wa kimataifa kinachoungwa mkono na umoja wa mataifa kikiongonzwa na maofisa wa polisi wa Kenya kilianza shughuli za kulinda Amani nchini humo kuanzia mwezi Juni. Kundi la Gran Grif limetajwa kuwa kundi baya Zaidi kwa kusababisha dhiki dhidi ya raia.
Kundi hilo limeshtumiwa kwa kutekeleza mauaji, ubakaji, wizi wa kimabavu na utekaji nyara, kulingana na ripoti ya umoja wa mataifa.
Mwanzilishi wa kundi hilo na kiongozi wake wa sasa wanakabiliwa na vikwanzo kutoka kwa Marekani.
Shambulizi hilo limejiri yapata mwezi mmoja tangu serikali ya mpito ya Haiti kutangaza hali ya kutotoka nje kote nchini humo.
Waziri mkuu Garry Conille ameahidi kukabili magenge huku umoja wa mataifa ukisema utumiaji nguvu kukabili magenge hayo unahitajika.