Takriban watu 61 wamefariki baada ya ndege walimokuwa wakisafiria kuanguka katika eneo la São Paulo nchini Brazil, kulingana na taarifa iliyotolewa na kampuni ya ndege ya Voepass.
“Tunasikitika kutangaza kuwa watu wote 61 waliokuwa ndani ya ndege hiyo nambari 2283 wamefariki katika ajali hiyo,” ilisema taarifa hiyo.
Kulingana na kanda za video zilizosambazwa mitandaoni, ndege hiyo inaonekana ikizunguka angani kabla ya kuanguka katika eneo la makazi.
Ndege hiyo inasemekana ilikuwa ikisafiri kutoka eneo la Cascavel katika jimbo la kusini la Paraná kuelekea uwanja wa ndege wa Guarulhos katika jiji la São Paulo, ajali hiyo ilipotokea.
Kulingana na taarifa ya kampuni hiyo ya Voepass, abiria wote ndani ya ndege hiyo walikuwa na stakabadhi kuonyesha ni raia wa Brazil. Hata hivyo haijabainika iwapo kuna abiria walikuwa na uraia wa nchi mbili.
Afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo Eduardo Busch, aliwaambia wanahabarti kwamba chanzo cha ajali hiyo bado hakijabainika.
“Wafanyakazi wote walikuwa wamehitimu,” alisema Busch.
“Tunasubiri mawasiliano katika ya rubani na kituo cha kuongoza safari za ndege, kufahamu kilichojiri,” aliongeza afisa huyo.