Watu 312 wamekamatwa kufuatia vurugu zilizoshuhudiwa jana Jumatano wakati wa maandamano yaliyoitishwa na muungano wa upinzani wa Azimio.
Mbunge wa Mavoko Patrick Makau ni miongoni mwa waliokamatwa kuhusiana na vurugu hizo.
Makau alikamatwa leo Alhamisi asubuhi katika makazi yake mtaani Karen kwa tuhuma za kupanga uharibifu mkubwa ulioshuhudiwa kwenye barabara ya Nairobi Expressway, katika kituo cha ulipiaji ada cha Mlolongo.
“Watu waliopanga moja kwa moja au isipokuwa moja kwa moja, kuchochea au kufadhili vurugu zilizoshuhudiwa jana Jumatano na vitendo vya uvunjaji wa sheria, akiwemo mbunge, wamekamatwa na watashtakiwa kwa makosa mbalimbali ya jinai,” amesema Waziri wa Usalama wa Taifa Kithure Kindiki wakati akifungua kituo cha polisi cha Kiserian na ofisi za kata ndogo ya Olosurutia katika eneo bunge la Kajiado Kaskazini, kaunti ya Kajiado.
“Msako wa wengine unaendelea. Vurugu zilizosababisha vifo, majeraha ya raia na maafisa wa usalama, utatizaji wa biashara za kila siku, uharibifu wa mali ya umma na binafsi, na visa vya uporaji ni vitendo vya uvunjaji sheria visivyoweza kukubalika au kutaihimilika.”
Huku akilaani maandamano hayo, Waziri Kindiki alisema hakuna uhusiano kati ya kupunguzwa kwa gharama ya maisha na uharibifu wa miundombinu muhimu ya nchi iliyojengwa kwa kutumia fedha za umma.
Kindiki sasa amewaelekeza maafisa wa usalama kutekeleza sheria kikamilifu na kukabiliana vilivyo na wahalifu wote wakiwemo wahujumu uchumi, waporaji na waharibifu wanaoharibu mali ya umma na ya kibinafsi.
Kauli zake zinawadia wakati ambapo Waziri wa Barabara na Uchukuzi Kipchumba Murkomen ameashiria kuwa gharama ya madhara yaliyosababishwa na maandamano ya hapo jana kwenye barabara ya Nairobi Expressway ni shilingi milioni 700.
Murkomen amesema waliosababisha uharibifu huo watagharimia uharibifu huo.