Watu ishirini wameripotiwa kuangamia baada ya mashua waliyokuwa wakisafiria kupinduka na kutumbukia katika Ziwa Victoria nchini Uganda.
Mashua hiyo ndogo inasemekana kuwabeba watu 34 wakati ajali hiyo ilipotokea jana Jumatano jioni huku watu 9 wakiokolewa.
Mashua hiyo ilikuwa pia imebeba magunia ya makaa, vyakula, samaki na mizigo mingine kwa mujibu wa ripoti za mwanzo, huku ikibainika kuwa ilizama kutokana na kubeba uzani kuzidi kiwango chake na pia hali mbaya ya hewa.
Wanajeshi wa Uganda wakishirikiana na wakazi wamekuwa wakitafuta watu waliopotea kufuatia mkasa huo tangu kutokea kwa ajali.