Home Habari Kuu Watu 174 walifariki kutokana na mvua za El Nino

Watu 174 walifariki kutokana na mvua za El Nino

0

Jumla ya watu 174 walifariki kutokana na mvua za El Nino zilizoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita. 

Kati ya waliofariki, watu 133 walikuwa watu wazima huku 41 wakiwa watoto.

Idadi ya familia zilizopoteza makazi imepungua hadi 15,208 katika kambi 79.

Awali, idadi ya familia zilizopoteza makazi ilikuwa 109,179 katika kambi 170.

Kwa mujibu wa kituo cha kamandi ya kitaifa ya kukabiliana na dharura na majanga ya mvua za El Nino, sekta ya kilimo pia iliathiriwa vibaya na mvua hizo huku mifugo 6,706 wakifariki hasa mbuzi na kondoo.

Mimea katika ekari zipatazo 84,568 pia iliharibiwa na kusababisha uharibifu wa jumla wa shilingi bilioni 16.26.

“Hii imekuwa na athari kubwa kwa kaunti kadhaa ikiwa ni pamoja na Lamu, Tana River, Garissa, Mandera, Wajir, Homa Bay na Kitui, na kusababisha tishio kubwa kwa usalama wa chakula,” kinasema kituo hicho katika taarifa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, juhudi zinaendelea kwa sasa kutoa misaada ya chakula kwa waathiriwa wa mvua hiyo huku miundombinu iliyoharibiwa ikikarabatiwa.

Hatua kubwa imepigwa katika kukarabati barabara ya Gamba-Witu katika kaunti ya Tana River na barabara ya Kona Punda – Mororo katika kaunti ya Garissa.

 

Website | + posts