Home Kimataifa Watu 120,000 wameajiriwa katika mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu

Watu 120,000 wameajiriwa katika mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu

0

Mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, umetoa fursa nyingi za ajira hapa nchini tangu kuanzishwa kwake.

Akihutubia taifa wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa taifa hili katika bustani ya Uhuru Jijini Nairobi, Rais William Ruto alisema mpango huo umetoa ajira za moja kwa moja na pia kufaidi pakubwa sekta za uzalishaji bidhaa za ujenzi.

Kulingana na kiongozi wa taifa, mpango huo ambao unatekelezwa katika maeneo 33 kote nchini, umesababisha ajira ya watu 120,000, huku walionufaika na mpango huo wakiwa wahandisi, wachoraji ramani, wataalam wa umeme na mafundi.

Rais alisema maeneo mengine 31 ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu yanafanyiwa ukaguzi, na ujezi utaanza mwezi Januari mwakani.

Alisema kufikia katikati ya mwaka 2024, ujenzi wa nyumba za gharama nafuu utatekelezwa katika kila kaunti hapa nchini.

“Lengo letu ni kujenga maelfu ya nyumba huku tukibuni nafasi za ajira. Mataifa ya Korea Kusini, Singapore na Malaysia yalianza mpango huu miaka 40 iliyopita, na sasa uchumi wa mataifa hayo umeshinda uchumi wa taifa hili,” alisema Rais Ruto.

Website | + posts