Home Kimataifa Watu 10 wakamatwa Singapore kwa kujipatia pesa kwa njia zisizo halali

Watu 10 wakamatwa Singapore kwa kujipatia pesa kwa njia zisizo halali

0

Maafisa wa polisi nchini Singapore wamekamata watu 10 na kutwaa mali ya thamani ya dola milioni 737, chini ya operesheni inayoendelea dhidi ya watu wanaoaminika kujipatia pesa kwa njia zisizo halali.

Maafisa wa polisi walitangaza jana Jumatano kwamba walitekeleza operesheni hizo kwa wakati mmoja kwenye makazi ya washukiwa ambapo walilenga watu ambao wanaaminika kujipatia pesa kutokana na uhalifu wa kupangwa katika nchi nyingine kama vile ulaghai wa mitandaoni na kamari ya mitandaoni.

Polisi walitwaa nyumba 94, magari ya kifahari 50, pesa taslimu, mikoba ya kifahari, vito vya thamani kubwa, vifaa vya kielekroniki, mvinyo, stakabadhi za umiliki wa mali kati ya vitu vingine vingi.

Waliokamatwa ni raia wa Uchina, Uturuki, Cambodia, Cyprus na Vanuatu na ni wa umri wa kati ya miaka 31 na 44.

Maafisa wa polisi wapatao 400 walihusika kwenye operesheni hizo na kukamata washukiwa kutoka makazi ya kifahari kote nchini Singapore.

Washuukiwa wanane bado wanasakwa na maafisa hao wa polisi huku 12 wakisaidia katika uchunguzi. Maafisa wanasema huenda watu wengine wakakamatwa, mali zaidi kutwaliwa na hata akaunti za benki kufungwa.

Nchi ya Singapore inafahamika ulimwenguni kote kuwa nchi ya uwekezaji na ina sheria kali za kudhibiti tabia ya watu kujipatia pesa kwa njia za udanganyifu.

Benki Kuu ya Singapore ilisema kwenye taarifa kwamba inaendeleza mawasiliano na benki ambazo zimesheheni pesa hizo ila haikuzitaja.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here