Home Habari Kuu Watoto watatu wafariki kwenye ajali Murang’a

Watoto watatu wafariki kwenye ajali Murang’a

0

Watoto watatu walidhibitishwa kufariki baada ya basi la shule kuanguka katika barabara ya kutoka Gitugi kuelekea mjini Murang’a Jumamosi jioni.

Ajali hiyo ilihusisha basi la shule ya chekechea ya Maadili ambayo iko mjini Thika kaunti ya Kiambu na ilitokea saa 12 jioni wanafunzi wakiwa njiani kutoka kaunti ya Nyeri.

Kamanda wa polisi katika kaunti ya Murang’a Kainga Mathiu anaelezea kwamba basi hilo lilikuwa limebeba wanafunzi 35 , madereva wawili na walimu watatu wakati wa ajali.

Kulingana na Kainga mtoto mmoja alifariki papo hapo na wengine wawili wakafariki wakipokea matibabu katika hospitali ya Murang’a Level Five.

Watoto wawili walioachwa na majeraha mabaya wamelazwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi huku wengine wakihudumiwa na kuruhusiwa kuondoka.

Basi hilo la shule lilipeleka watoto na walimu kuhudhuria hafla ya chama cha maskauti huko Nyeri na ajali ilitokea wakirejea Thika.

Eneo la ajali linafahamika sana kwa matukio sawia na liko kilomita chache tu kutoka mjini Murang’a , lina kona kali ambayo imesababisha waendeshaji magari wengi kuanguka katika muda wa miezi michache iliyopita.