Watoto 12 pamoja na watu wengine wazima wameuawa kwenye shambulizi la roketi katika eneo la Golan linalokaliwa na Israel. Haya ni kwa mujibu wa maafisa.
Roketi hiyo ilipata wahasiriwa kwenye uwanja wa kabumbu na kulingana na jeshi la Israel, ilirushwa na kundi la Lebanon Hezbollah madai ambayo kundi hilo linakataa.
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kulipiza kisasi shambulizi hilo akiongeza kwamba ‘watalipa kwa gharama kubwa’.
Tukio hilo kulingana na wadadisi huenda likazua vita vikali Tkati ya Israel na kundi la Hezbollah, ambao wamefyatuliana risasi awali wakati wa vita vya Israel katika ukanda wa Gaza.
Shambulizi hilo la Jumamosi ndilo baya zaidi kuwahi kutekelezwa katika eneo la kaskazini mwa Israel tangu vita vya Gaza vilipoaza Oktoba 7, 2023.
Taarifa ya umoja wa mataifa ilisema kwamba hatua ya kujizuia ni muhimu kwa pande zote kwani kuna tishio la mgogoro mkubwa ambao unaweza kuathiri eneo zima.
Msemaji wa kundi la Hezbollah Mohamad Afif alikanusha madai kwamba kundi hilo lilitekeleza shambulizi la Golan Heights huku taarifa zikijiri kwamba mlipuko ulisababishwa na roketi ya Israel.
Kulingana na Israeli waliouawa walikuwa kati ya umri wa miaka 10 na 20.
Video iliyosambazwa mitandaoni ilionyesha umati wa watu kwenye uwanja huo wa kandanda huku machela na ambulensi vikielekezwa huko.