Watoto sita wameaga dunia kwenye mkasa wa moto mashariki ya DR Congo baada ya moto kuzuka kwenye kambi moja ya wakimbizi wa ndani kwa ndani.
Kambi hiyo iko katika mji wa Kalehe na ni makazi ya familia zipatazo 420 kutoka kijiji cha Bushushu karibu na ziwa Kivu kwenye mpaka kati ya nchi hiyo na Rwanda. Walipoteza makazi yao kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi.
Mvua kubwa iliyosababisha janga hilo ilinyesha Mei, 2023, na kusababisha vifo vya watu wapatao 400 wakati huo.
Moto ulizuka kwenye kambi hiyo Jumamosi jioni na kuua wavulana wawili na wasichana wanne wa umri wa kati ya mwaka mmoja na miaka minne.
Thomas Bakenga, msimamizi wa eneo la Kalehe alielezea pia kwamba watu wazima wanne wamelazwa hospitalini kutokana na majeraha waliyopata kwenye mkasa huo.
Moto huo ulianzia kwenye nyumba moja katikati ya kambi wakati mtoto mmoja alikuwa akiandaa chakula bila uwepo wa wazazi wake.
Nyumba zilizoezekwa kwa nyasi na kuta za karatasi za plastiki zipatazo 360 ziliharibiwa kwenye moto huo mkali.
“Tulijaribu kuwaokoa lakini hakukuwa na matumaini. Moto uliharibu kila kitu.” alisema Bakenga.
Msimamizi wa kundi moja la kutetea haki za kibinadamu kwa jina Delphin Birimbi, anaomba serikali ya Congo na mashirika yasiyo ya kiserekali yasaidie waathiriwa.
Afisi ya umoja wa mataifa kuhusu usaidizi wa jamii inakadiria kwamba kufikia sasa familia 3000 zimepoteza makazi kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi.