Home Habari Kuu Watendakazi wa Huduma Kenya wafanya matembezi Nairobi

Watendakazi wa Huduma Kenya wafanya matembezi Nairobi

0

Watendakazi wa vituo vya Huduma Kenya walifanya matembezi kwenye barabara za jiji la Nairobi katika msafara wa kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja.

Wiki ya huduma kwa wateja mwaka huu wa 2023 inaadhimishwa kuanzia Oktoba 2 hadi 6.

Wakiongozwa na mkurugenzi mtendaji Ben Kai Chilumo, wakiwa wamevalia mavazi ya rangi nyeupe yenye nembo za Huduma Kenya na wakiwa wameandamana na bendi ya spick and span ya polisi, watendakazi hao walipitia barabara za Nairobi kuanzia jumba la Harambee.

Katibu katika idara ya utendakazi wa umma Amos Gathecha, ndiye alianzisha msafara huo nje ya jumba la Harambee saa tatu unusu asubuhi.

Gathecha alisisitiza kwamba huduma bora kwa wateja ni haki yao ya kikatiba akiahidi kwamba serikali itawaunga mkono kikamilifu watendakazi wa shirika la Huduma Kenya ambao alisema wanatekeleza jukumu muhimu katika kutoa huduma muhimu za serikali.

Katibu wa masuala ya jinsia Veronica Nduva alipongeza vituo vya Huduma kote nchini kwa kuanzisha vituo vidogo vya ushauri nasaha na kutoa huduma hizo pia kupitia mitandao akisema huduma hiyo inasaidia katika kupunguza visa vya dhuluma za kijinsia na kinyumbani.

Aliahidi kuendelea kusaidia shirika la Huduma ili kuhakikisha kwamba wakenya wengi zaidi wanapata huduma za ushauri nasaha.