Home Habari Kuu Watahiniwa wa KCPE 2023 waanza kujiunga na kidato cha kwanza

Watahiniwa wa KCPE 2023 waanza kujiunga na kidato cha kwanza

0

Maelfu ya watahiniwa waliofanya mtihani wa darasa la nane, KCPE mwaka 2023 wameanza kujiunga na kidato cha kwanza. 

Vituo vya magari vilifurika wanafunzi walioonekana kuwa na bashasha wakati wakielekea kujiunga na shule walizoitwa na ambazo zitakuwa makao yao kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu, wakati akiongoza zoezi la uteuzi wa wanafunzi hao Disemba 18, 2023 alisema anatarajia wanafunzi wote waliofanya mtihani huo kujiunga na shule za upili.

Jumla ya wanafunzi 42,927 waliteuliwa kujiunga na shule za kitaifa, 22,051 wakiwa wavulana na 20,876 wakiwa wasichana.

Wanafunzi 288,201 waliteuliwa kujiunga na shule za kaunti, kati yao 129,332 wakiwa wavulana na 158,869 wakiwa wavulana.

Kwa upande mwingine, jumla ya wanafunzi 274,746 waliteuliwa kujiunga na shule za Extra County, 141,590 wakiwa wavulana na 133,156 wakiwa wasichana.

Wanafunzi 2,225 waliteuliwa kujiunga na shule zenye mahitaji maalum, 1,214 wakiwa wavulana na 1,011 wasichana.

Idadi kubwa ya watahiniwa watajiunga na shule za kaunti ndogo baada ya jumla ya wanafunzi 792,230 kuteuliwa kujiunga na shule hizo, 423,171 wakiwa wavulana huku 369,059 wakiwa wasichana.

“Katika uteuzi huo, watahiniwa wote waliopata alama 400 na zaidi waliwekwa katika shule za kitaifa au za Extra County,” alisema Waziri Machogu aliyesisitiza kuwa uteuzi uliambatana na chaguo la mwanafunzi na taratibu zingine.

“Vile vile, watahiniwa wengine wote waliwekwa katika shule za kaunti au kaunti ndogo, kulingana na vigezo vilivyowekwa. Wanafunzi wenye mahitaji maalum waliwekwa ama katika shule za kawaida au zenye mahitaji maalum kwa kuzingatia kategoria zao za ulemavu, ustahili au chaguo.”

 

Website | + posts