Home Kaunti Wasiwasi watanda Chepareria baada ya nyumba kadhaa kuchomwa

Wasiwasi watanda Chepareria baada ya nyumba kadhaa kuchomwa

Familia kadhaa zililazimika kulala nje kwenye kibaridi huku nyingine zikitafuta hifadhi kwa majirani baada ya nyumba zao kuchomwa na watu wanaoaminika kuwa wahuni wa kukodishwa katika kijiji cha Tampalal kaunti ndogo ya Chepareria, kaunti ya Pokot Magharibi.

Mzozo wa ardhi unaaminika kuchochea hali hiyo ambapo waathiriwa wanadai kusikia milango yao ikibishwa kwa fujo jana Jumamosi alfajiri na watu waliokuwa wakipiga kelele wakisema wanataka kuchoma nyumba zao.

Mmoja wa waathiriwa Kochepchumba Beatrice alielezea kwamba aliamshwa na watu asiowajua saa nane usiku akatolewa nje pamoja na wanawe na wajukuu.

watu hao walimwagia nyumba zake tatu petroli na kuwasha moto na kisha kutoroka na kujificha kwenye msitu ulio karibu.

Beatrice alipoteza mali yake yote kwenye kisa hicho vikiwemo vyeti vya masomo vya watoto wake na stakabadhi nyingine muhimu.

Faith Chepkemei ambaye pia aliathirika alisema kwamba wavamizi hao ambao anakisia walikuwa zaidi ya 50 walikuwa wamejipanga vilivyo kwani hawakuwapa muda hata wa kuokoa chochote.

Waathiriwa wameachwa wasijue cha kufanya huku wakihofia maisha yao kwani wahuni hao huenda wakawavamia tena kwa sababu ya mzozo wa ardhi.

Inaarifiwa kwamba mzozo huo umekuwepo kwa miaka 48 sasa na kwamba watu zaidi ya elfy 3 kwenye shamba kubwa la Tampalal huko Chepareria waliathiriwa na uvamizi huo.

Kesi kuhusu ardhi hiyo inaendelea mahakamani na wanashangaa ni kwa nini wamelazimika kukosa makazi ilhali hawakupatiwa ilani ya kuhama eneo hilo.

Wanaomba viongozi wa eneo hilo kuingilia kati kesi inayoendelea na kuwasaidia kupata mahitaji ya msingi kama chakula, mavazi makazi na hata ulinzi.

Naibu kamanda wa polisi wa eneo hilo Adano Abukula alielezea kwamba familia za eneo hilo ambazo zilikuwa zimekimbilia mahakama zilishindwa kwenye kesi hiyo na kulikuwa na mipango ya kuondoa watu hao kwenye ardhi hiyo.

Kulingana na Adano ilani ya kuwaondoa ilitolewa mwaka jana lakini haikuwa imetekelezwa kwani wanafuata taratibu zilizoko.

Inaaminika kwamba walioshinda kesi wamekosa subira na kuamua kuchukua sheria mkononi huku akisema uchunguzi umeanzishwa.