Home Kaunti Wasimamizi wa mitihani wasifiwa kwa utendakazi bora

Wasimamizi wa mitihani wasifiwa kwa utendakazi bora

Dkt. Kipsang alitoa wito kwa wasimamizi wa vituo vya mitihani, wakaguzi na maafisa wa usalama kutolegea hadi mtihani utakapokamilika.

0

Serikali imeweka mikakati kabambe kuhakikisha uadilifu unazingatiwa katika mitihani ya kitaifa.

Katibu wa elimu ya msingi, Dkt. Belio Kipsang, amesema kufikia sasa hakuna visa vikubwa vya utovu wa nidhamu ukiwemo udanganyifu ambavyo vimeripotiwa tangu mitihani hiyo kuanza wiki mbili zilizopita.

Katibu huyo alihusisha hili na ushirikiano wa asasi mbalimbali katika kusimamia mitihani hiyo huku akiwapongeza walimu na vyombo vya usalama kwa juhudi zao za kuhakikisha mtihani unafanywa bila matatizo.

Akizungumza katika eneo la Kisumu ya Kati kwenye ziara ya ukaguzi wa usimamizi wa mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne,KCSE, Dkt. Kipsang alitoa wito kwa wasimamizi wa vituo vya mitihani, wakaguzi na maafisa wa usalama kutolegea hadi mtihani utakapokamilika.

Aliwataka wasimamizi wa vituo vya mitihani na shule kujiepusha na vishawishi vya kuruhusu udanganyifu wakati wa mitihani hiyo.

Aidha alisema wizara ya elimu iko mbioni kutekeleza mapendekezo ya jopokazi la elimu lililobuniwa na rais.

Website | + posts