Washukiwa wawili wanaohusishwa na mauaji ya afisa mmoja wa polisi katika eneo la Hawinga, kaunti ya Siaya mapema wiki, wameuawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi.
Ikithibitisha kisa hicho, huduma ya taifa ya polisi ilisema bunduki mbili zilizokuwa zimeibwa pia zilipatikana.
“Bunduki aina ya MP5 na AK47, zilipatikana katika eneo la Hawinga katika nyumba ya Sheikh Rashid aliyetoroka mtego wa polisi,” ilisema huduma ya taifa ya polisi.
Siku ya Jumatatu juma hili, maafisa wawili wa polisi waliokuwa wakisindikiza karatasi za mtihani wa KCSE eneo la Alego Usonga, katika kaunti ya Siaya, walishambuliwa na wahalifu wawili waliokuwa wamejihami kwa visu.
Washambuliaji hao waliwapora maafisa hao bunduki zao zilizokuwa na jumla ya risasi 60.
Maafisa wa usalama katika kaunti ya Siaya wakiwahutubia wanahabari walisema kuwa maafisa hao walishambuliwa baada ya kushuka kwenye basi moja ambalo halingeweza kuingia kwenye shule ya sekondari ya Mahero, kutokana na hali duni ya barabara.
Mwalimu mmoja hata hivyo alinusurika alipokimbilia usalama wake akiwa na karatasi za mtihani.