Maafisa wa polisi wamewakamata washukiwa wawili wakiwa na vifaa vinavyoshukiwa kuwa vilipuzi, katika kaunti ya Kisii.
Wilfred Chaha Mokami mwenye umri wa miaka 28 na Chabere Mwita Mahenda mwenye umri wa miaka 49, walikuwa wakiendesha gari lenye usajili KDQ 445R na lori lenye usajili ZH 4943, waliposimamishwa na maafisa wa polisi.
Kupitia ukurasa wa X, idara ya kukabiliana na makosa ya jinai DCI, ilisema baada ya upekuzi, maafisa wake walipata vipande 459 vya vilipuzi na viunganishi vya kufanikisha ulipuzi.
Washukiwa hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Mosocho, huku maafisa hao wa upelelezi wakiendelea na uchunguzi.
Vilipuzi hivyo pamoja na magari hayo pia yanazuiliwa na yatatumika kama ushahidi.