Home Kaunti Washukiwa wawili kushtakiwa kwa mauaji ya mwanablogu Daniel Muthiani

Washukiwa wawili kushtakiwa kwa mauaji ya mwanablogu Daniel Muthiani

Upande wa mashtaka umebaini kuwepo kwa ushahidi wa kutosha kuwafungulia shtaka la mauaji wawili hao.

Washukiwa wawili waliohusishwa na mauaji ya mwanablogu wa Meru Daniel Muthiani Benard almaarufu Snipper watashtakiwa kwa mauaji.

Afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma ameagiza Vincent Mureithi Kirimi almaarufu Supuu na Murangiri Kenneth Guantai almaarufu Tali wafikishwe mbele ya Mahakama kuu mjini Kiambu kwa shtaka la mauaji.

Kupitia taarifa, mkurugenzi wa mashtaka ya umma amesema baada ya uchunguzi wa matukio, upande wa mashtaka umebaini kuwepo kwa ushahidi wa kutosha kuwafungulia shtaka la mauaji wawili hao.

Mmoja wa washtakiwa hao ni nduguye Gavana wa Meru Kawira Mwangaza.

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma pia amewasilisha kesi dhidi ya washukiwa wengine watano inayoshughulikiwa katika mahakama ya Kibera.

Mwanablogu huyo wa Meru aliripotiwa kupotea tarehe mbili mwezi Disemba mwaka jana, huku mwili wake ukipatikana umetupwa katika mto Mutonga kaunti ya Tharaka Nithi tarehe 16 mwezi huo wa Disemba.