Maafisa wa polisi wamemtia nguvuni mshukiwa mkuu katika mauaji ya afisa wa idara ya upelelezi wa jinai, DCI David Mayaka, yaliyotekelezwa wiki iliyopita katika mtaa wa Kayole.
Alex Wanjiru alikamatwa akiwa katika eneo la Ruthingiti, kaunti ya Kiambu na maafisa wa DCI kutoka Nairobi.
“Alex Wanjiru mwenye umri wa miaka 23, aliyekuwa miongoni mwa genge lililotekeleza mauaji ya afisa wa polisi David Mayaka, alitoroka kutoka Kayole baada tu ya kutekeleza mauaji hayo na kuelekea nyumbani kwa nyanya yake eneo la Ruthingiti, kaunti ndogo ya Kikuyu kabla ya kufumaniwa na maafisa wa polisi,” ilisema taarifa ya DCI.
Kulingana na maafisa wa polisi, washukiwa saba wanaohushishwa na mauaji ya Mayaka wametiwa nguvuni.
Kundi hilo linalochunguza mauaji ya Constable David Mayaka, pia limenasa pikipiki iliyotumiwa kutekeleza uhalifu huo yenye nambari za usajili KMGJ 350V.
Mmoja wa washukiwa alikamatwa katika eneo la Kikuyu alikokuwa amejificha ilhali wengine walikamatwa katika maeneo ya Kayole na Githurai.
Maafisa hao wa DCI pia wamehusisha bunduki iliyotumiwa na wahalifu hao na visa vingine vitano vya ujambazi katika jiji la Nairobi.
Aidha polisi wanasaka washukiwa wengine wawili, Henry Njihia anayeaminika kufyatua risasi iliyomuua Mayaka na John Kamau almaarufu Faruk, ambaye amejihami kwa bastola aina ya glock.
Kundi la makachero hao limesema liliwakamata washukiwa wa mauaji hayo baada ya kuchunguza maganda ya risasi mahali Mayaka aliyekuwa afisa wa DCI Makadara alipouawa.
Mkewe marehemu Mayaka, Hellen Kemunto amelazwa hospitalini baada ya kupigwa risasi kwenye paja la kushoto.
Afisa huyo aliuawa alipokuwa akibadilisha gurudumu la gari lake katika tukio lililonaswa na kamera za CCTV.