Home Habari Kuu Washukiwa wa wizi wa kimabavu wakamatwa

Washukiwa wa wizi wa kimabavu wakamatwa

Kulingana na taarifa ya polisi, washukiwa hao walikamatwa katika eneo la kwa Vonza kaunti ya Kitui, baada ya gari moja kuripotiwa kuibwa kaunti ya Machakos.

0
Washukiwa wa wizi wa kimabavu wakamatwa.

Maafisa wa polisi wamewakamata washukiwa wanne wa wizi wa kimabavu, ambao hutekeleza uovu huo katika kaunti za Machakos na Makueni.

Kulingana na taarifa ya polisi, washukiwa hao walikamatwa katika eneo la Vonza kaunti ya Kitui, baada ya gari moja kuripotiwa kuibwa katika kaunti ya Machakos.

Uchunguzi wa polisi umebainisha kuwa washukiwa hao George Maloba Osokho, Martin Nyamai, Edward Rogova Mudachi na Morris Muli Lumumba, wana rekodi za uhalifu na walishtakiwa awali katika mahakama moja ya Machakos kwa wizi wa kimabavu.

Aidha, uchunguzi huo pia umegundua kwamba washukiwa hao ni sehemu ya genge la majambazi ambalo hutekeleza uhalifu kati ya Nairobi, Mlolongo, Machakos, Makueni na kwenye mpaka wa Kenya na Tanzania, ambapo magari ya wizi huuzwa.

Kwa mujibu wa maafisa wa polisi, washukiwa hao hukodisha magari wakidai yanatumika katika sherehe za harusi au shughuli za kampuni, lakini hutoweka na magari hayo.

Kesi dhidi yao zinasubiri kusikizwa katika mahakama za Makueni na Machakos.

Website | + posts