Home Habari Kuu Washukiwa wa ulaghai wa dhahabu wanaswa Kileleshwa, Nairobi

Washukiwa wa ulaghai wa dhahabu wanaswa Kileleshwa, Nairobi

0

Washukiwa kadhaa wanaoshukiwa kujihusisha katika sakata kubwa ya dhahabu wamenaswa katika mtaa wa Kileleshwa, kaunti ya Nairobi. 

Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI inasema washukiwa katika sakata hiyo waliwalenga raia wawili wa Malaysia.

Wakati wa operesheni kali iliyoendeshwa na makachero wa DCI, vifaa mbalimbali vilivyotumiwa katika ulaghai huo uliotibuliwa vilipatikana.

Kwa mujibu wa DCI, operesheni hiyo ilianzishwa kufuatia taarifa za kijasusi zilizopokelewa na Afisa wa Upelelezi wa Jinai, OSU katika kaunti ndogo ya Kilimani kuhusu njama ya kuwalaghai raia hao wawili wa Malaysia.

Kufuatia taarifa hizo, OSU alituma timu ya upelelezi baada ya raia wa Malaysia kuwasili nchini.

Iliripotiwa kuwa walaghai walikuwa wamewasiliana na raia hao kuanzia Octoba 19, 2023 kupitia mitandao ya kijamii wakidai kuwauzia kilo 500 za dhahabu yenye thamani ya dola milioni 19 za Marekani ambazo ni sawa na shilingi bilioni 2.85 za Kenya.

Katika makubaliano kati yao, raia hao wa Malaysia walikuwa tayari wametuma dola 6,350 kwa wanachama wa genge hilo waliopo nchini Cameroon ambao waliwaelekeza kwa wanachama wenzao nchini Kenya.

Walaghai hao walifuatiliwa wakati wakiwachukua raia hao wa Malaysia kutoka hotelini kwenye barabara ya Argwings Kodhek mtaani Kilimani wakitumia gari aina ya Toyota Noah, nambari za usajili KCW 835U.

Walaghai waliwapeleka raia hao katika afisi iliyo katika nyumba ya kibinafsi kwenye barabara ya Mageta mtaani Kileleshwa ambako timu ya upelelezi ilifuatilia mambo kwa karibu kabla ya lango kuu kufungwa na kuifungia nje.

Baadhi ya washukiwa waliruka ua na kukwepa msako wa maafisa wa upelelezi waliofanikiwa kuingia uani kwa kutumia uweledi wa kazi yao.

Washukiwa 7 walikamatwa huku wengine 2 wakifanikiwa kutoroka.

Washukiwa hao wanaojumuisha walinzi wawili wa kampuni ya G4S ni pamoja na Didier Muke, Brian Otiende, Patrick Otieno, Joshua Ngandi, Charles Vincent Njerenga, na Mark Kabete na Ken Kiboi wanaofanya kazi na kampuni ya G4S.

Washukiwa watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.

Website | + posts