Home Habari Kuu Washukiwa wa mauaji ya mwanariadha Benjamin Kiplagat kufanyiwa uchunguzi wa akili

Washukiwa wa mauaji ya mwanariadha Benjamin Kiplagat kufanyiwa uchunguzi wa akili

Maafisa wa polisi walipata kisu kinachoaminika kuhusika katika mauaji hayo ya mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 34.

0

Washukiwa wawili wa mauaji ya mwanariadha Benjamin Kiplagat, watafanyiwa uchunguzi wa akili kabla ya kujibu mashtaka ya mauaji yanayowakabili.

Mahakama moja ya Eldoret ilitoa agizo kwamba washukiwa hao David Ekai, almaarufu Timo mwenye umri wa miaka 25  na Peter Khalumi mwenye umri wa miaka 30, wapelekwe katika hospitali ya rufaa na mafunzo ya Moi, kubainisha hali yao ya afya ya akili.

Naibu msajili wa mahakama kuu ya Eldoret Rosemary Onkoba, aliagiza wawili hao wazuiliwe katika gereza la Eldoret kabla ya kufikishwa mahakamani tarehe 31 mwezi Januari mwaka 2024, ili kushtakiwa kwa mauaji.

Wawili hao ambapo mmoja ni mhudumu wa bodaboda, walitiwa nguvuni kwa kuhusishwa na mauaji ya mwanariadha Benjamin kiplagat, aliyepatikana amedungwa kisu ndani ya gari lake katika mtaa wa Kimumu kwenye barabara kuu ya Eldoret-Iten highway, kaunti ya Uasin Gishu.

Maafisa wa polisi walipata kisu kinachoaminika kuhusika katika mauaji hayo ya mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 34.

kulingana na maafisa wa usalama, mauaji hayo huenda ni kisa cha wizi, kwa kuwa washukiwa hao walimuibia pesa na simu ya mkononi.

Kiplagat anatoka katika kaunti ya Elgeyo Marakwet na ni mwanariadha wa nne kuuawa katika eneo hilo.

Miongoni mwa wanariadha ambao wamepoteza maisha yao katika eneo hilo ni pamoja na bingwa mara mbili wa dunia wa mbio za cross-country Agnes Tirop, aliyeuawa miaka mitatu iliyopita na mume wake Ibrahim Rotich. mwili wa Damaris Muthee ulipatikana nyumbani kwa mwanariadha wa Ethiopia miaka miwili iliyopita, huku mwanariadha wa Rwanda Rubayit Siragi, akiuawa mjini Iten, katika kile polisi walitaja kuwa ghasia za kimapenzi.