Home Habari Kuu Washukiwa katika mlipuko wa gesi Embakasi wafikishwa mahakamani

Washukiwa katika mlipuko wa gesi Embakasi wafikishwa mahakamani

Hadi kufikia sasa watu sita wamefariki kutokana na mlipuko huo wa gesi, uliotokea wiki jana, huku wengine 300 wakijeruhiwa.

0
Washukiwa wa mlipuko wa gesi Embakasi.

Washukiwa wanne wanaohusishwa na mlipuko wa gesi uliotokea eneo la Embakasi juma lililopita, walifikishwa katika mahakama moja ya Milimani.

Wanne hao wanajumuisha Derrick Kimathi ambaye ni mmiliki wa kituo hicho cha kuuza gesi, David Ongare,Joseph Makau na Mirrian Kioko  ambao ni maafisa wa halmashauri ya usimamizi wa mazingira NEMA.

Upande wa mashtaka uliiomba mahakama iwazuilie washukiwa hao ili kuwapa maafisa wa polisi muda wa kukamilisha uchunguzi. Kimathi alizuiliwa katika kituo cha polisi cha  Embakasi baada ya kujisalimisha jana.

Idara ya DCI imesema bado inawatafuta washukiwa wengine watano.Washukiwa hao ni pamoja na Stephen Kilonzo, ambaye ni msimamizi wa eneo la kituo hicho, Ann Kabiri Mirungi na Lynette Cheruiyot wa NEMA, dereva wa lori Robert Gitau na dereva mwingine aliyetambuliwa kuwa Abraham Mwangi.

Hadi kufikia sasa watu sita wamefariki kutokana na mlipuko huo wa gesi, uliotokea wiki jana, huku wengine 300 wakijeruhiwa.

Kisa hicho cha alhamisi kilitokea baada ya lori lililokuwa limebeba mitungi ya gesi kulipuka mwendo wa saa tano unusu usiku na kusababisha moto mkubwa.

Website | + posts