Home Habari Kuu Washukiwa 7 wafikishwa mahakamani kwa kukwepa kulipa ushuru

Washukiwa 7 wafikishwa mahakamani kwa kukwepa kulipa ushuru

0

Washukiwa wengine 7 wamefikishwa kwenye mahakama ya Milimani leo ambapo walishtakiwa kwa kosa la kukwepa kulipa ushuru wa shilingi milioni 6.7 katika uagizaji wa maziwa ya unga.

Saba hao Amhed Ibrahim, Osama Abdikarim, Abdimalik Mohamed, Abdiwahid Osman, said Abdulahi, Dahir Hussein na Nabusuwa, walifikishwa mbele ya hakimu mkuu Benard Ochoi.

Washukiwa hao walikamatwa katika mtaa wa Eastleigh jijini Nairobi baada ya kupatikana na mikebe elfu 7284 na magunia 7 ya maziwa hayo ya unga bila kibali cha uagizaji kutoka nje wala ithibati ya kulipa ushuru.

Bidhaa hiyo ilitwaliwa kutoka kwa duka la jumla la Amana katika jumba la Moyale mtaani Eastleigh.

Washukiwa walikana mashtaka na wakaachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni mbili kila mmoja au dhamana ya pesa taslimu ya shilingi laki 5 kila mmoja.

Kesi yao itatajwa Februari 7, 2024.

Jumla ya watu ambao wamekamatwa kwa kukwepa kulipa ushuru katika uagizaji wa maziwa ya unga mwezi huu wa Januari ni 15.

Dahir Amhed Hassan na Abdifitah Amhed Dahir walikamatwa Januari 16, 2024 katika duka la Safacom mtaani Eastleigh na magunia 408 ya maziwa ya unga ambayo hayakuwa yamelipiwa ushuru.

Walifikishwa mahakamani Milimani Januari 17, 2024, kwa kukwepa kulipa ushuru wa shilingi milioni 6.

Wengine 6 walikamatwa Januari 9 kwa biashara hiyo hiyo mtaani Eastleigh na sasa mamlaka kukusanya ushuru nchini KRA inashirikiana na asasi nyingine za serikali kupambana na biashara haramu.

Website | + posts