Mfanyabiashara Jimi Wanjigi amedai kukamatwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI.
Wanjigi alifika katika ofisi za DCI eneo la Nairobi leo Jumatatu mchana ili kuandikisha taarifa kuhusiana na madai ya kufadhili maandamano yaliyoshuhuiwa nchini siku chache zilizopita.
“DCI imenikamata kinyume cha sheria licha ya kutolewa kwa maagizo mengi yanayozuia kukamatwa kwangu,” alisema Wanjigi kupitia mtandao wa X.
Ripoti zinaashiria kuwa Wanjigi atazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kamukunji akisubiri kufikishwa katika mahakama Kuu ya Milimani kesho Jumanne.
Matamashi yake yanakuja siku chache baada ya Mahakama Kuu Agosti 16 mwaka huu kuongeza muda wa agizo la kutokamatwa kwa mfanyabiashara huyo ambaye pia si mgeni katika ulingo wa kisiasa.
Kwenye uamuzi wake, Jaji Bahati Mwamuye aliongeza muda wa kuzuia kukamatwa kwa Wanjigi hadi Septemba 19.
Hata hivyo, mahakama haikutoa vikwazo dhidi ya Wanjigi kufunguliwa mashtaka mapya.
Kesi hiyo itatajwa tena Septemba 19 mwaka huu.
Wanjigi amekwaruzana na maafisa wa polisi katika siku za hivi karibuni kwa tuhuma kuwa amekuwa akifadhili maandamano ya vijana wa Gen Z, madai ambayo amekanusha vikali.
Siku chache zilizopita, maafisa wa polisi walivamia nyumbani kwake wakitaka kumkamata ila hawakumpata.
Ni hatua iliyomlazimu Wanjigi kukimbilia mamlaka na kupata agizo la kuzuia maafisa wa polisi kumkamata.
Wanjigi amekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Kenya Kwanza anaoutuhumu kwa kuyumbisha uchumi wa nchi.