Home Habari Kuu UN: Wanawake na wasichana wameathirika zaidi na uvamizi wa mfumo wa afya...

UN: Wanawake na wasichana wameathirika zaidi na uvamizi wa mfumo wa afya Sudan

0

Shirika la Afya Duniani, WHO na lile la UNFPA ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa, UN linaloshughulikia afya ya uzazi jana Jumatano yalionya kwamba uvamizi unaoendelea dhidi ya vituo vya afya, vifaa na wahudumu wa afya nchini Sudan unazuia wanawake na wasichana kupata huduma za matibabu za kuokoa maisha, wajawazito wakiathirika zaidi.

Asilimia 67 ya hospitali zote za maeneo yanayoshuhudia mapigano zimefungwa na hospitali nyingi za kina mama kujifungulia hazifanyi kazi ikiwemo hospitali kubwa ya rufaa nchini sudan ya Omdurman.

Kati ya watu milioni 11 wanaohitaji huduma za afya kwa dharura nchini Sudan, wapo wanawake na wasichana milioni 2.64 ambao wako katika umri wa kupata watoto.

262, 880 ni wajawazito na elfu 90 watajifungua katika muda wa miezi mitatu ijayo. Wote hao wanahitaji huduma muhimu za afya ya uzazi.

Tangu mapigano yalipoanza mwezi Aprili, WHO imethibitisha visa 46 vya mashambulizi dhidi ya wahudumu wa afya na vifaa ambapo watu 8 waliuawa na 18 kujeruhiwa.

Vifaa na mali nyingine za mfumo wa afya zimeibwa na wahudumu wa afya kuelekezewa vurugu.

Ripoti zinaashiria kwamba jeshi la Sudan linakalia mabohari ya hazina ya kitaifa ya vifaa vya matibabu, NMSF jijini Khartoum, ambapo dawa za nchi nzima uhifadhiwa.

Vifaa vya matibabu ya dharura vya shirika la WHO pia vinahifadhiwa kwenye mojawapo ya mabohari hayo.

Hospitali hazina mafuta ya kuwasha majenereta yanayotoa umeme hali iliyosababisha vifo vya watoto sita waliokuwa wamezaliwa katika hospitali moja mjini Eld’aeen mashariki ya Darfur katika muda wa wiki moja.

Madaktari wanasema kwamba yamkini watoto 30 wamefariki katika hospitali hiyo tangu mapigano yalipozuka.

Mkurugenzi Mkuu wa UNFPA Dr. Natalia Kanem anasema mapigano ni sharti yakome, hospitali zilindwe na wahudumu wa afya na wagonjwa pia walindwe.

Anasema misaada ya kibinadamu nayo lazima iruhusiwe.

Juzi Jumanne, mkutano wa mawaziri wanne wa shirika la IGAD uliamua kwamba mkutano wa ana kwa ana na viongozi wa pande zinazozozana nchini Sudan ni muhimu katika kuafikia amani ya kudumu na kuendeleza mabadiliko ya amani hadi kwa demokrasia na uongozi wa raia nchini humo.

Mkutano huo chini ya uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Dr. Alfred Mutua uliafikia kwamba mkutano na viongozi wa pande mbili nchini Sudan urahisishe mambo kama vile kukomeshwa kwa vita na kuruhusu usafirishaji wa misaada kwa raia wanayoihitaji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here