Home Habari Kuu Wanaofuja fedha za NHIF chuma chao ki motoni, asema Rais Ruto

Wanaofuja fedha za NHIF chuma chao ki motoni, asema Rais Ruto

Kiongozi wa taifa, alisema Serikali imejipanga kufanikisha huduma ya Afya kwa Wote (UHC).

0

Rais William Ruto ametoa onyo kali kwa wanaofuja fedha za umma ndani ya Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Hospitali (NHIF).

Alidai kuwa Serikali haitavumilia majaribio ya watu wachache, ya kuhujumu mfumo wa NHIF na kupora rasilimali zake kwa maslahi kibinafsi.

Kiongozi huyo wa taifa, alisema Serikali imejipanga kufanikisha huduma ya Afya kwa Wote (UHC), na kupunguza michango ya kila mwezi kwa watu wa kipato cha chini.

“Hatutakubali kudanganywa kwa sababu wanaofadhili kesi mahakamani dhidi ya UHC ni watu wanaonufaika na ufisadi katika NHIF,” alisema.

Rais William Ruto wakati wa mnada wa mbuzi na utamaduni wa Kimalel kaunti ya Baringo.

Akiongeza: “Tutawafichua wote na kuhakikisha kile tunachofanya katika sekta ya afya kinatolewa kwa manufaa ya mamilioni ya Wakenya.”

Rais aliyasema hayo Siku ya Alhamisi, wakati wa mnada wa mbuzi na utamaduni wa Kimalel kaunti ya Baringo.

Wengine waliokuwepo ni naibu Rais Rigathi Gachagua, mawaziri Kipchumba Murkomen, Simon Chelugui, Gavana wa Baringo Benjamin Cheboi na mwenzake wa Elgeiyo Marakwet Wesley Rotich na wabunge miongoni mwa viongozi wengine.

Kwa upande wake, naibu Rais Rigathi Gachagua, alisema utawala unaoongozwa na Rais Ruto umeweka mikakati thabiti kurejesha uchumi wa nchi.

Hata hivyo, aliwataka Wakenya kuwa na subira na kuipa serikali nafasi ya kutimiza ajenda yake ya maendeleo.