Home Habari Kuu Wanajeshi wahusishwa katika usaidizi wa waathiriwa wa mafuriko

Wanajeshi wahusishwa katika usaidizi wa waathiriwa wa mafuriko

0

Wizara ya usalama wa taifa imetangaza kwamba wanajeshi sasa wanahusika katika shughuli za kutafuta na kuokoa walioathiriwa na mafuriko.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari leo, wizara hiyo ilielezea kwamba wanajeshi wapatao 151 wanatoa usaidizi katika eneo la Maai Mahiu kaunti ya Nakuru ambapo miili 52 imepatikana huku watu 51 wakiwa hawajulikani waliko.

Vijana 400 kutoka huduma ya vijana kwa taifa NYS pia wanahusika katika harakati za uokoaji huko Maai Mahiu na Talek ambapo mto Talek ulivunja kingo zake na kusababisha mafuriko katika hoteli 19 zilizo kwenye mbuga ya Maasai Mara.

Watu 90 waliokolewa kutoka kwenye hoteli hizo na hakuna vifo vilivyoripotiwa. Kituo cha ufuatiliaji kimewekwa katika lango la Sekenani la mbuga ya Maasai Mara.

Kufikia sasa kaunti 28 zimeathiriwa na mafuriko zikiwemo,Kakamega, Vihiga, Busia, Bungoma, Trans Nzoia,Kisumu, Kisii, Nyamira, Migori, Siaya, Homabay, Nandi, Bomet, Nakuru, Elgeyo Marakwet, West Pokot, Baringo, Uasin Gishu na Narok.

Katika eneo la kati mwa nchi kaunti zilizoathirika ni pamoja na Nyeri, Muranga, Kirinyaga, Kiambu na Laikipia huko mashariki mwa nchi Embu, Tharaka Nithi na Meru ndizo zimeathirika.

Kaunti ya Nairobi nayo haijasaazwa na kwa jumla watu 196,296 wameathiriwa na mafuriko kote nchini.

Utathmini wa mabwawa unaendelea katika sehemu mbali mbali za nchi huku mabwawa 192 yanayosemekana kuwa katika hatari kubwa ya kuporomoka yakiangaziwa zaidi.

Wahisani wamehimizwa kuendelea kusaidia waathiriwa hasa katika kaunti za Nairobi, Kirinyaga, Homabay na Tana River.

Hali ya anga katika eneo la kaskazini Mashariki inaonekana kuboreka na hivyo kusaidia kuimarisha mipango ya kurejesha hali ya kawaida baada ya mafuriko.

Website | + posts