Pande zinazozozana nchini Sudan ambazo ni jeshi la taifa hilo na kundi la Rapid Support Forces, RSF zimekubaliana kusitisha mapigano kwa muda wa siku tatu kuanzia leo Jumapili, Juni 18.
Haya ni kwa mujibu wa wapatanishi wa Marekani na Saudi Arabia.
Makubaliano hayo yataanza kutekelezwa saa kumi jioni na kuendelea hadi Juni 21.
Haya yanajiri wakati ambapo mapigano yameshika kasi hasa katika jiji kuu la Khartoum.
Marekani na Saudi Arabia wamekuwa wakijaribu kupatanisha pande zinazozozana kwa wiki kadhaa sasa na majarabio ya awali ya kuafikia mapatano ya kusitisha mapigano hayajafua dafu.
Badala yake mapigano yamekuwa yakiongezeka.
Kulingana na taarifa iliyotolewa Jumamosi, Juni 17, wawakilishi wa jeshi la Sudan na wa kundi la RSF walikubaliana kusitisha mapigano kwa siku tatu na hakuna kundi ambalo litatumia muda huo kujiendeleza kivita. Muda huo utatoa fursa pia ya kusafirishwa kwa misaada ya kibinadamu kote nchini Sudan.
Wapatanishi wametishia kusitisha mazungumzo ya kutafuta kumaliza vita yanayoendelea jijini Jeddah iwapo pande hizo mbili hazitatii mapatano hayo ya kusitisha mapigano kwa siku tatu.
Kesho Jumatatu kutaandaliwa mkutano wa kuchangisha fedha za kufadhili misaada ya kibinadamu nchini Sudan ambapo watu wapatao milioni 25 sawa na nusu ya idadi ya watu nchini humo wanahitaji misaada na ulinzi.
Mapigano kati ya jeshi la Sudan na kundi la RSF yalizuka katikati ya mwezi Aprili mwaka huu kutokana na kutoelewana kwa viongozi wao Abdel Fattah al-Burhan na Mohamed Hamdan Daglo.