Home Kimataifa Wanajeshi kuhusishwa kwa shughuli za kusafisha jiji la Dar es Salaam

Wanajeshi kuhusishwa kwa shughuli za kusafisha jiji la Dar es Salaam

0

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania Albert Chalamila ametangaza kwamba wanajeshi wa taifa hilo watahusishwa kwenye shughuli za kusafisha jiji hilo.

Akizungumza katika hafla ya kutawaza viongozi wa kanisa la Baptist jijini Dar es Salaam, Chalamila alisema hatua hiyo ilichochewa na kuzuka kwa ugonjwa wa kipindupindu katika mikoa 6.

Kulingana naye, hata ingawa Dar es Salaam haijaathirika, wameona ni vyema wafanye usafi.

“Kwa hivyo mkiona wanajeshi wengi barabarani msiogope, mjue wanafanya usafi jijini Dar es Salaam,” alisema Chalamila kuhusu shughuli hiyo itakayofanyika Januari 23 na 24 mwaka huu wa 2024 katika wilaya zote za mkoa huo.

Wanajeshi hao watasaidiwa na maafisa wengine wa ulinzi wakiwemo polisi wa kawaida.

Wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam wamehimizwa pia kuwa mabalozi wa usafi ili kuepusha magonjwa kama kipindupindu.

Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA  Freeman Mbowe naye ametangaza maandamano Januari 24, 2024 nchini humo kama njia ya kushinikiza serikali kusikiliza maoni kuhusu uundaji wa tume huru ya uchaguzi.

Watanzania wanatizamiwa kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu mwaka ujao wa 2025.