Kituo cha radio cha Thome FM na mashabiki wake kinaomboleza vifo vya watangazaji wake wawili waliofariki kwenye ajali ya barabarani katika soko la Riandira lililo kwenye barabara ya Sagana-Makutano kaunti ya Kirinyaga.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Mwea, ‘’Stephen Waigwa wa umri wa miaka 21 alikuwa amembeba Caroline Kamunya wa umri wa miaka 20 kwa pikipiki. Walipofika kwenye kanisa la Riandra SDA, walinuia kuingia upande wa kulia na ni hapo walipogongwa na gari aina ya Probox’’ alisema Ali.
Wawili hao walifariki papo hapo huku dereva wa gari hilo na abiria wake wakipata majeraha mabaya na kukimbizwa hospitalini.
Mkuu wa kituo hicho kinachopeperusha matangazo kupitia mtandao- Mwangi wa Wangu, mauti yaliwakumba wawili hao baada ya sherehe ya miaka minne ya kituo hicho mjini Kutus. ‘’tulishinda pamoja kwa njia ya furaha na wasikilizaji wetu tukisherekea miaka minne ya kituo chetu, jioni, wawili hao waliondoka kuenda maombi kanisani ila tukapokea simu kuwa wamepata ajali’’ alisema Mwangi.
Pia aliwataja kuwa limbukeni wenye vipaji vikuu vya utangazaji.
Miili ya wawili hao ilipelekwa katika makavazi ya hospitali ya Kerugoya kwa upasuaji.