Home Kaunti Wanahabari Meru washirikiana na kundi la kutunza mazingira kupanda miti

Wanahabari Meru washirikiana na kundi la kutunza mazingira kupanda miti

0

Baraza la vyombo vya habari nchini tawi la kaunti ya Meru, chama cha wanahabari Meru na kundi la kutunza mazingira katika kaunti ya Meru wameshirikiana katika juhudi za kuhakikisha upanzi wa miche 500 ya miti ya matunda katika taasisi za elimu za kaunti hiyo.

Akizungumza wakati wa upanzi wa miche hiyo katika shule ya msingi ya Meru, meneja wa baraza la vyombo vya habari nchini eneo la mlima Kenya Jackson Karanja alisema kwamba ushirikiano huo unadhamiriwa kuhakikisha kwamba wahusika wote katika tasnia ya vyombo vya habari wanachangia katika kutekeleza azimio la Rais William Ruto la upanzi wa miti.

Karanja alisema kwamba kando na jukumu lao la msingi la kukusanya habari, wanahabari wana jukumu la kuhakikisha wanatunza mazingira.

Alielezea kwamba miche hiyo 500 ya miti ya matunda itafaidi shule tatu za eneo hilo ambazo ni shule ya msingi ya Meru, Shule ya msingi ya mtakatifu Paulo na shule ya msingi ya Meru Muslim. Lengo kuu alisema ni kuhakikisha wanafunzi wanapata matunda ya kula wakiwa shuleni siku za usoni.

Katibu wa chama cha wanahabari cha Meru almaarufu “Meru press club – MPC” Anthony Miriti naye alisema wanafurahia kama chama kushirikiana na baraza la vyombo vya habari katika mpango huo wa kutunza mazingira.

Aliahidi kwamba wanachama wa MPC watajihusisha na juhudi za kutunza mazingira huku wakielemisha jamii kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na kutoa changamoto kwa wanahabari katika sehemu nyingine nchini kuiga mfano huo.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Meru Eva Gichuru alishukuru baraza la vyombo vya habari na chama cha wanahabari katika kaunti ya Meru kwa mpango wao wa kupanda miche ya miti ya matunda shuleni.

Alisema mpango huo utahimiza wanafunzi kuelewa umuhimu wa kutunza mazingira.

Website | + posts