Home Habari Kuu Wanagenzi walipwe mshahara, mswada wapendekeza

Wanagenzi walipwe mshahara, mswada wapendekeza

0
kra

Mbunge wa Samburu Magharibi Naisula Lesuuda amewasilisha mswada bungeni ambao unapendekeza kuwa wanagenzi katika ofisi za umma walipwe mshahara na kupewa siku za mapumziko.

Alipokuwa akiwasilisha mswada wa wanagenzi wa umma mbele ya Bunge la Kitaifa mnamo Jumanne, Lesuuda alisisitiza hitaji la kuwa na mfumo wa kisheria unaolenga kushughulikia masaibu ya wanagenzi nchini.

kra

Mbunge huyo alisema alipokea mapendekezo ya kujumuisha sekta ya kibinafsi na kuhakikisha kuwa wanagenzi wanawekwa kwenye mazingira yenye hadhi.

Hata hivyo, Lesuuda alisema pia alipokea wasiwasi kwamba hatua hiyo huenda ikapelekea kampuni za kibinafsi kuwanyima nafasi wanagenzi hao.

“Tunahitaji kulitafakari vizuri ili tuweze kushirikisha sekta binafsi jinsi wanavyoweza kuwashirikisha wanagenzi na kuhakikisha kuwa wanatendewa kwa utu, wanapewa mshahara,” alisema Lesuuda.

Wakati huo huo, Lesuuda alipendekeza kuwa serikali iwawezeshe makampuni katika sekta ya kibinafsi ili kuwaruhusu kuwalipa mshahara wanagenzi.

Mswada huo unalenga kudhibiti programu za mafunzo kwa wahitimu wa vyuo vya kadri na vyuo vikuu ndani ya utumishi wa umma.

Iwapo mswada huo utapitishwa, utawapa wahitimu wasio na ajira ujuzi ufaao ambao wanahitaji uzoefu wa vitendo, au wahitimu wenye sifa za kitaaluma ambao wanatakiwa na mashirika ya kitaaluma kufanya mafunzo ya kazi kama sharti la kusajiliwa.

Pia, itatumika kwa mtu yeyote ambaye amehitimu mafunzo ya kozi kwa ufanisi chini ya Sheria ya Mafunzo ya Ufundi na Vyuo vya Ufundi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here