Wanafunzi wote waliofanya mtihani wa darasa la nane, KCPE wa mwaka huu wa 2023 watajiunga na shule za upili.
Hii ilibainika leo Jumatatu wakati Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alipoongoza hafla ya uteuzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2024 katika shule ya upili ya Lenana jijini Nairobi.
Kwa mujibu wa uteuzi huo, jumla ya wanafunzi 42,927 wameteuliwa kujiunga na shule za kitaifa, 22,051 wakiwa wavulana na 20,876 wakiwa wasichana huku jumla ya wanafunzi 2,225 wakiteuliwa kujiunga na shule zenye mahitaji maalum, 1,214 wakiwa wavulana na 1,011 wasichana.
Wanafunzi 274,746 wameteuliwa kujiunga na shule za Extra County, 141,590 wakiwa wavulana na 133,156 wakiwa wasichana huku jumla ya wanafunzi 288,201 wakiteuliwa kujiunga na shule za kaunti, kati yao 129,332 wakiwa wavulana na 158,869 wakiwa wavulana.
Kwa upande mwingine, idadi kubwa ya watahiniwa watajiunga na shule za kaunti ndogo baada ya jumla ya wanafunzi 792,230 kujiunga na shule hizo, 423,171 wakiwa wavulana huku 369,059 wakiwa wasichana.
“Katika uteuzi huo, watahiniwa wote waliopata alama 400 na zaidi waliwekwa katika shule za kitaifa au za Extra County,” alisema Waziri Machogu aliyesisitiza kuwa uteuzi uliambatana na chaguo la mwanafunzi na taratibu nyiingine.
“Vile vile, watahiniwa wengine wote waliwekwa katika shule za kaunti au kaunti ndogo, kulingana na vigezo vilivyowekwa. Wanafunzi wenye mahitaji maalum waliwekwa ama katika shule za kawaida au zenye mahitaji maalum kwa kuzingatia kategoria zao za ulemavu, ustahili au chaguo.”
Wanafunzi wataanza kujiunga na shule walizoteuliwa Januari 15 mwakani.