Home Habari Kuu Wanafunzi wa vyuo vikuu wahimizwa kushiriki upanzi wa miti

Wanafunzi wa vyuo vikuu wahimizwa kushiriki upanzi wa miti

Dorcas aliwahamasisha wanafunzi hao dhidi ya utumizi wa mihadarati na unywaji wa pombe.

0
Mke wa naibu rais, Mchungaji Dorcas Rigathi.

Mke wa naibu Rais mchungaji  Dorcas Rigathi, ametoa wito kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kote nchini, kujihusisha na shughuli ya upanzi wa miti, kuambatana na lengo la serikali la kupanda miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032.

Akizungumza alipoongoza wanafunzi wa chuo kikuu cha Chuka kupanda miti 8,000, Dorcas alisema upanzi wa miti zaidi, utakabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

“Natoa wito kwa vyuo vikuu, kutenga ardhi ili wanafunzi wakuze miche ya miti, na nitashirikiana nao,”alisema mchungaji Dorcas.

Mbunge wa eneo hilo Patrick Munene, aliwapongeza wananfunzi hao kwa kushiriki zoezi la upanzi wa miti.

“Mtaacha kumbukumbu ya kupigiwa mfano katika taasisi hii, kupitia zoezi hili la upanzi wa miti,”alisema Munene.

Upanzi huo wa miti ulitekelezwa ili kuafikia lengo la upanzi wa miti milioni mbili na afisi ya naibu Rais, ambayo imebuni afisi ya mke wa naibu Rais.

Upanzi huo wa miti ulifanywa baada ya kukamilika kwa mkutano kati ya mke huyo wa naibu Rais na wanafunzi wa chuo kikuu cha Chuka.

Katika mkutano huo, Dorcas aliwahamasisha wanafunzi hao dhidi ya utumizi wa mihadarati na unywaji wa pombe.

Mchungaji Dorcas amekuwa na mikutano sawia na hiyo katika vyuo vikuu kadhaa hapa nchini, katika juhudi za kuwarai vijana kusitisha unywaji wa pombe na matumizi ya mihadarati.