Home Vipindi Wanafunzi maskini Bomet wanufaika na ufadhili wa masomo

Wanafunzi maskini Bomet wanufaika na ufadhili wa masomo

0

Serikali ya kaunti ya Bomet imetoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 250 werevu lakini kutoka familia maskini katika kaunti hiyo.

Wanafunzi hao ni miongoni wale watakaojiunga na kidato cha kwanza wiki ijayo.

Wanafunzi wengine 625 wanatarajiwa kujiunga na vyuo vya mafunzo ya kiufundi ili kupata ujuzi utakaohakikisha wanapata kipato maishani.

Akitangaza kutolewa kwa ufadhili huo, Gavana Prof. Hillary Barchok alisema utawala wake umetenga shilingi milioni 141 kwa shule mbalimbali na vyuo vya mafunzo ya kiufundi ili kugharimia karo kwa wanafunzi watakaonufaika na ufadhili huo.

“Wakati mtakaporipoti shuleni wiki ijayo, natoa changamoto kwenu kufuata nyayo za Emmanuel Kipkoech ambaye pia alinufaika na ufadhili huo na ambaye ametufanya tujivunie kwa kupata Gredi ya A katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, KCSE wa mwaka 2023,” Gavana Barchok alitoa wito kwa wanafunzi watakaonufaika na ufadhili huo.

Alipongeza Kamati ya Msaada wa Masomo ya Wadi na ile ya Msaada wa Masomo ya Kaunti kwa kufanya kazi maridhawa katika uteuzi wa wanafunzi watakaonufaika na ufadhili huo wa masomo akitaja zoezi la uteuzi kuwa la kukuna kichwa.

Aidha alizipongeza benki za Equity, KCB, Cooperative na Family miongoni mwa washirika wengine kwa kuunga mkono juhudi za kaunti hiyo kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi watakaojiunga na shule za upili mwaka huu.

Aliwataka wanafunzi watakaonufaika na ufadhili huo kutia bidii masomoni aliyosema yana nguvu ya kubadilisha dira ya maisha ya mtu yeyote yule.

Website | + posts