Wanafunzi 70 wa shule ya Hillside Endarasha kaunti ya Nyeri, hawajulikani waliko baada ya moto kuteketeza moja ya mabweni ya shule hiyo na kusababisha vifo vya wanafunzi 18.
Naibu Rais Rigathi Gachagua, alithibitisha hayo, alipokuwa akiwahutubia waandishi wa habari alipozuru shule hiyo Ijumaa alasiri.
Kulingana na Gachagua, wanafunzi 37 wameunganishwa na familia zao na wengine 27 wanapokea matibabu hospitalini.
Moto huo ulitokea katika bweni lililokuwa na vitanda 156, lililowahifadhi wanafunzi wa kiume pekee katika shule hiyo ya bweni ya kibinafsi.
Aidha idadi kamili ya wanafunzi waliokuwa katika bweni hilo wakati wa mkasa huo, haijabainika, lakini wanafunzi 86 wamebainishwa walipo.
Alitoa wito wa utulivu huku serikali ikianzisha uchunguzi kubainisha chanzo cha moto huo.