Home Habari Kuu Wamiliki wa matatu wapinga pendekezo la kuweka kamera kwenye magari yao

Wamiliki wa matatu wapinga pendekezo la kuweka kamera kwenye magari yao

Rais wa chama cha wamiliki wa magari ya uchukuzi wa abiria nchini Matatu owners Albert Karakacha amesema kwamba wamiliki wa magari hayo hawakubaliani na pendekezo la wizara ya uchukuzi la kuweka kamera kwenye magari yao.

Akizungumza mjini Meru kwenye mkutano wa viongozi wa chama cha wamiliki wa Matatu na wamiliki wa matatu wa kaunti za Meru na Isiolo, Karakacha alisema wamiliki wa Matatu wangependa kuona madereva wakipunguza ajali barabarani na wanatizamia kuafikia hilo kupitia kuanzisha shule yao ya uendeshaji gari na wanataka wizara ya uchukuzi iwasaidie kuafikia ndoto hiyo.

Karakacha anaamini kwamba kuweka kamera kwenye magari hayo hakutapunguza ajali kwa vyovyote kwani hata baada ya kubadili vidhibiti mwendo mara tano ajali bado zinashuhudiwa.

Patrisiah Musimi ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa chama hicho cha wamiliki wa Matatu alifafanua kwamba mkutano huo mjini Meru ulikusudiwa kukulisha wanachama viongozi wapya.

Bi Musyimi alisema pia kwamba wanataka kutumia mikutano hiyo kote nchini kukusanya maoni kutoka kwa wanachama ili kusaidia kurejesha utulivu katika sekta ya Matatu nchini.

Titus Mwiti ambaye ni mwenyekiti wa tawi la Meru la chama hicho cha wamiliki wa Matatu alishukuru viongozi wa kitaifa kwa kuwazuru.

Alisema wamiliki wa Matatu Meru wanashirikiana na gavana wa kaunti hiyo na idara ya polisi wa trafiki, mamlaka ya kitaifa ya usalama NTSA na mashirika mengine ya serikali kuhakikisha mazingira bora ya kuhudumu.

Website | + posts
Jeff Mwangi
+ posts