Home Kaunti Waliotoroka mafuriko Garissa wahimizwa kurejea nyumbani

Waliotoroka mafuriko Garissa wahimizwa kurejea nyumbani

Kambi nyingi za wakimbizi zilikuwa katika shule za msingi, ambapo waathiriwa wamekuwa wakiishi huko kwa majuma matatu yaliyopita.

0

Kamishna wa kaunti ya Garissa Solomon Chesut, amewahimiza waliotoroka makwao kutokana na mafuriko ya mvua za El Nino kurejea makwao, baada ya viwango vya maji kupungua.

Kambi nyingi za wakimbizi zilikuwa katika shule za msingi, ambapo waathiriwa wamekuwa wakiishi huko kwa majuma matatu yaliyopita.

Akizungumza wakati wa sherehe ya Jamhuri siku ya Jumanne, Chesut aliishukuru serikali ya kaunti hiyo, washirika wa maendeleo na serikali ya kitaifa kwa juhudi zao za kuokoa maisha wakati wa mafuriko yaliyoshuhudiwa katika kaunti hiyo.

Zaidi ya familia 30,000 katika kaunti hiyo ziliathirika, hususan wale wanaioshi karibu na mto Tana ambao ulivunja kingo zake na kusababisha uharibifu mkubwa katika mashamba na vituo vilivyokuwa karibu.

“Shule zitafunguliwa Katika muda wa majuma mawili au matatu yajayo, na watu wanapaswa kujitayarisha kurejea nyumbani kwani viwango vya maji vimepungua. Tutawasaidia na magodoro, vyandarua vya kuzuia mbu na bidhaa zingine za msimu ili warejee nyumbani,” alisema Chesut.

Kwa upande wake gavana wa Garissa Nathif Jama alishukuru shirika la mpango wa chakula duniani kwa kutoa ndege ili kusaidia katika usambazaji wa chakula cha msaada kwa waathiriwa wa mafuriko katika maeneo ya kaunti hiyo ambapo barabara zilikuwa hazipitiki.

Website | + posts