Idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye mkasa wa mafuriko katika mji wa Derna nchini Libya huenda ikafikia 20,000.
Kulingana na vyanzo vya habari nchini humo, zaidi ya watu 5,000 wamethibitishwa kufariki huku wengine wapatao 10,000 wakiwa hawajulikani waliko.
Mafuriko hayo yalisomba kijiji kizima Jumapili iliyopita usiku baada ya mabwawa mawili kupasuka kufuatia mvua kubwa iliyoandamana na kimbunga kwa jina Daniel.
Waokoaji wanaendelea kutafuta miili baada ya matumaini ya kuwapata manusura kudidimia.