Jamaa wa wahasiriwa 47 waliofariki wakati wa mkasa wa kupasuka kwa bwawa la Solai, wameafikiana na mmiliki wa bwawa hilo kuhusu mpango wa kuwafidia.
Hii ni baada ya malumbano ya muda mrefu mahakamani.
Tume ya Kutetea Haki za Kibinadamu, KHRC ilikuwa mpatanishi kwenye maafikiano hayo ya nje ya mahakama.
Pande zote mbili zilikubaliana kuhusu fidia ya shilingi milioni 1.2 kwa mtu mzima na shilingi 800,000 kwa watoto waliofariki.
Mkasa huo ulitokea mwaka 2018 wakati bwawa hilo lilipopasuka na kusababisha mafuriko katika shamba moja la kahawa la ekari 3,000 na kuharibu makazi ya watu wengi.
Watu 47 walithibitishwa kufariki na maelfu ya wengine kuachwa bila makao katika vijiji jirani vya Energy, Nyakinyua, Endao, Arutani, na Milmet.
Kwenye kesi hiyo, wamiliki wa bwawa hilo walikabiliwa na tuhuma za uhalifu ikiwemo kutozingatia taratibu za ujenzi wa bwawa.
Mwezi Aprili mwaka huu, Hakimu Mkuu wa Naivasha Nathan Lutta aliamua kuwa mmiliki wa bwawa hilo alikuwa na kesi ya kujibu.