Waziri wa mazingira Aden Duale ameamuru taasisi za kibinafsi na za umma ambazo paa zao zimeezekwa kwa bidhaa zilizoundwa kwa kutumia madini ya Asbestos waziondoe.
Duale ametoa makataa ya miezi mitatu kwa sehemu hizo za umma kubadili paa zao la sivyo zichukuliwe hatua za kisheria kwa kuhatarisha maisha ya wananchi.
Madini ya Asbestos yanahusishwa na kutoshika joto na kutopata kutu ndiposa yanatumiwa kwa wingi katika kuunda “Tiles” ambazo hutumika kuezeka nyumba badala ya mabati.
Hatari ya madini hayo ni iwapo yatapumuliwa na binadamu yanabakia kwenye mapafu kwa miaka mingi na kuyaathiri na huenda pia yakasababisha saratani.
Kenya ilipiga marufuku matumizi ya madini hayo mwaka 2006.
Siku chache zilizopita, waziri Duale aliomba idara ya mahakama isaidie katika utekelezaji wa marufuku hiyo kama njia ya kulinda maisha ya wananchi.
Akizungumza wakati wa kuzinduliwa kwa mpango wa kujumuisha utunzaji mazingira katika idara ya sheria nchini, Duale alisema changamoto za kimazingira zinazoshuhudiwa nchini zinatokana na kukosa kutekeleza sheria zilizopo.
Waziri huyo alihimiza wadau wote wa mazingira ikiwemo mamlaka inayosimamia mazingira nchini NEMA kushirikiana kutunza mazingira kote nchini.