Home Habari Kuu Walimu wataka usimamizi wa hazina ya malipo yao ya kustaafu uhamishwe

Walimu wataka usimamizi wa hazina ya malipo yao ya kustaafu uhamishwe

Walimu kupitia chama chao cha KNUT sasa wanataka usimamizi wa hazina yao ya malipo ya kustaafu uondolewe kutoka kwa wizara ya fedha na kuwekwa chini ya tume ya kuajiri walimu nchini TSC.

Katibu mkuu wa chama cha KNUT Collins Oyuu ambaye alifika mbele ya kamati ya bunge kuhusu elimu, aliwataka wabunge kubadili sheria iliyobuni tume ya kuajiri walimu nchini TSC.

Mabadiliko hayo ni kwa lengo la kuhakikisha kwamba TSC inakabidhiwa usimamizi wa malipo ya kustaafu ya walimu.

Chama hicho kinataka wabunge pia kuangazia tena pendekezo la walimu wanaostaafu kuendelea kupokea mshahara wa kila mwezi hadi watakapopata malipo yao ya kustaafu.

Oyuu alikuwa amefika mbele ya kamati ya bunge kuhusu elimu kujibu maswali yaliyoibuliwa na kamati hiyo kama vile masharti ya mwalimu kupatiwa wadhifa wa mwalimu mkuu wa taasisi ya elimu.

Maswali mengine ni pamoja na idadi ya walimu waliohudumu kwa kandarasi kwa zaidi ya miezi 6, mapendekezo ya utekelezaji wa mchakato wa kupandisha walimu vyeo, orodha ya walimu waliohamishiwa Junior Secondary ila mshahara wao haukubadilishwa na orodha ya walimu 1000 waliopatiwa majukumu ya kusimamia taasisi za elimu bila nyongeza ya mshahara.

KNUT ilikuwa imeulizwa pia kuhusu idadi ya wanachama wake katika kila kaunti na kiasi cha pesa chama hicho kinakusanya kutoka kwa wanachama kila mwezi.

Website | + posts
Kevin Wachira
+ posts