Home Vipindi Walimu wa JSS waapa kutorejea darasani hadi serikali itekeleze mahitaji yao

Walimu wa JSS waapa kutorejea darasani hadi serikali itekeleze mahitaji yao

Walimu wa shule za sekondari msingi yaani Junior secondary schools JSS wameapa kutorejea darasani hadi pale ambapo serikali itakaposhughulikia matakwa yao.

Wakizungumza mjini Olkalou katika kaunti ya Nyandarua walikoandaa maandamano, walimu hao waliokuwa na hasira walisema kwamba mshahara ambao wamekuwa wakipokea ni kidogo na haukidhi mahitaji yao hasa wakati huu ambao ushuru wa bidhaa za kimsingi umeongezwa pamoja na ushuru wanaotozwa kama ushuru wa nyumba.

Wanasema kwamba muda wa masharti waliyoajiriwa kwayo ya uanagenzi umekwisha kwani ni mwaka wa pili sasa na serikali iliahidi kuwaajiri kwa masharti ya kudumu ahadi ambayo bado haijatimia.

Walilalamikia kile walichokitaja kuwa ripoti za hatua ya baadhi ya wabunge na wanasiasa kugawa barua za ajira katika mikutano ya kisiasa.

Mmoja wa walimu hao wa JSS katika kaunti ya Nyandarua Emma Muthoni, aliiomba serikali isikie kilio chao kwani wengi wao ni wazazi ambao lazima wakidhi mahitaji ya familia zao.

Walimu hao wanadai pia fidia ya miezi 12 ambayo wamekuwa wakitoa huduma kama walimu ambayo wanasema ni shilingi elfu 480, kwa kila mmoja na waajiriwe kwa masharti ya kudumu.

Website | + posts
Lydia Mwangi
+ posts