Home Habari Kuu Walemavu wapatiwa viungo bandia Meru

Walemavu wapatiwa viungo bandia Meru

Watu 140 ambao walipoteza miguu na mikono katika mazingira tofauti katika kaunti ya Meru, wamepokea viungo bandia kwa hisani ya Hindu Samaj Meru, shirika kutoka India likishirikiana na mbunge wa Imenti Kaskazini Rahim Dawood.

Dkt. Vinod Ramji wa shirika la Hindu Samaj, alisema viungo hivyo bandia vitasaidia wanaovihitaji ili maisha yao yawe ya kawaida na waweze kutekeleza shughuli zao za kila siku bila matatizo mengi.

Alisema walionelea wapatie watu ambao wanahitaji viungo hivyo bandia kama njia ya kusaidia wasiojiweza katika jamii.

Dawood alisema viungo hivyo vimetolewa bila malipo yoyote na sio watu wa kaunti ya Meru pekee wamefaidi bali pia watu wa kaunti jirani.

Mbunge huyo alisema atawasiliana na Waziri wa Afya nchini kuona iwapo viungo hivyo bandia havitatozwa ushuru ili watu wengi zaidi wafaidi kutokana na msaada huo kutoka India.

Easter Gacheri na Friday Kananu ambao ni wakazi wa kaunti ya Meru, walishukuru shirika la Hindu Samaj na mbunge Rahim Dawood kwa kuleta madaktari wa shirika hilo la Narayan kusaidia watu wanaohitaji viungo bandia vya mwili.

Wawili hao waliridhika baada ya kupokea miguu bandia ambayo itawasaidia sana baada ya kusumbuka kwa muda kutembea na kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Website | + posts
Jeff Mwangi
+ posts