Home Kaunti Wakulima Trans Nzoia kugawiwa mbegu za alizeti

Wakulima Trans Nzoia kugawiwa mbegu za alizeti

0

Wakulima katika kaunti ya Trans Nzoia watagawiwa mbegu za alizeti chini ya mpango uliozinduliwa jana na Gavana wa kaunti hiyo George Natembeya.

Mpango huo ni ushirikiano kati ya serikali ya kaunti hiyo na kampuni ya Kenya seed na unalenga kupanua wigo wa ukulima katika eneo hilo na kupunguza utegemezi wa zao la mahindi.

Akizungumza wakati wa kuzindua usambazaji huo Natembeya alisema wakulima wa eneo hilo wameangazia sana ukuzaji mahindi kwa kiwango cha asilimia 80 lakini sasa wana fursa ya kuongeza zao jingine.

Chini ya mpango huo wakulima watapatiwa mbegu za alizeti pamoja na mafunzo kuhusu jinsi ya kukuza zao hilo.

Serikali ya kaunti ya Trans Nzoia itasaidia katika kuongeza thamani zao hilo na kutafuta soko.

Anaamini ukulima wa alizeti una uwezo wa kubuni nafasi za ajira na kuimarisha uchumi wa nchi hii. Alisema pia kwamba mmea wa alizeti ni himilivu na unaweza kusaidia wakulima kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Lengo letu ni kuona kwamba ukulima wa alizeti unafanywa kwenye ekari 100,000 katika muda wa miaka mitano ijayo.” alisema Natembeya na kuongeza kwamba amejitolea kuhakikisha ufanisi wa mradi wa kuimarisha mafuta ya kupikia.

Eneo la kukusanyia bidhaa na viwanda linalojengwa katika kaunti ya Trans Nzoia alisema litasaidia sana kwani litakuwa na vifaa vya kuongeza thamani kwenye mazao kando na kuwapa wakulima wadogo uwezo wa kuafikia thamani kubwa kutoka kwa mazao yao.

Gavana Natembeya alishukuru mamlaka ya kilimo na chakula, kampuni ya mbegu Kenya Seed na wadau wengine kwa kuunga mkono mradi wa mafuta ya kupikia.

Aliahidi kuchangia ongezeko la ardhi inayotumia kukuza mimea ya mafuta ya kupikia kutoka ekari elfu 60, hadi ekari elfu 250 katika muda wa miaka mitano ijayo.

Website | + posts