Wakulima zaidi ya 1,000 wa Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Kahawa cha Kikima katika eneo la Mbooni kaunti ya Makueni wameahidi kurejelea shughuli zao za ukulima wa kahawa.
Wakulima hao walitoa ahadi hiyo wakati wa hafla ya kupokea mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 4.7 iliyotolewa na Hazina ya Cherry.
Wakulima hao sasa wanasema wako tayari kurudi shambani na kufanya ukulima wa kahawa.
Wametaja changamoto zilizokuwa zikiwakabili na kusababisha kusimamisha uzalishaji wa zao hilo ikiwa ni pamoja na matatizo ya mawakala wa kahawa ambao wamekuwa kikwazo kwao.
Charles Mutwiri ni Mkurugenzi wa chama kipya cha Kenya Planters Co-operative Union (New KPCU). Amewahimiza wakulima wa kahawa kuzingatia uzalishaji wa kahawa bora kabla ya kulalamikia masoko na pia kusisitiza umuhimu wa kuwa na mazao bora ili kuvutia masoko na kuongeza mapato.
Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Jr. alielezea kusikitishwa kwake na malipo duni na unyanyasaji unaofanywa na mawakala wa kahawa kwa wakulima.
Aliwahakikishia wakulima kuwa serikali yake itafanya kazi kuhakikisha wanapata mbolea na dawa za kutosha ili kuongeza uzalishaji wao na kuboresha maisha yao.
Mwakilishi Wadi wa eneo hilo Alexander Mulemba alisema kuwa bunge la eneo hilo linapanga kupitisha bajeti ya milioni mbili katika wadi mbili zinazohusika na wakulima wa kahawa. Hii itasaidia wakulima 1,200 kupata miche 100 kila mmoja.
Wakulima hao sasa wanatarajia kurejelea shughuli zao za ukulima wa kahawa na wana matumaini makubwa ya kufanikiwa.
Haya yanajiri wakati Naibu Rais Rigathi Gachagua amewasili nchini Colombia akiandamana na wakulima wa kahawa kutoka Kenya kuangazia namna ya kuifufua sekta hiyo wakati pia wakitafuta masoko bora ya kuuza zao hilo.