Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi, COTU umesitisha kimya chake na kumtetea Brian Mwenda Njagi kutokana na madai ya kuhudumu kama wakili bila ya kutimiza vigezo vinavyohitajika kuhudumu katika wadhifa huo.
Chama cha wanasheria nchini, LSK tawi la Nairobi kilikuwa cha kwanza kuutaarifu umma kuwa Njagi amekuwa akisingizia kuhudumu kama wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya na isitoshe kudai kuwa mwanachama wa chama hicho wakati yeye si wakili.
“Tawi hili lingependa kuutarifu umma kuwa Brian Mwenda Njagi siyo wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya, kwa kuzingatia rekodi za chama, na wala si mwanachama wa tawi la Nairobi,” kilisema chama cha LSK katika taarifa yake wakati kikitoa wito kwa umma kuwaripoti mawakili bandia ili hatua mwafaka ichukuliwe dhidi yao.
Chama hicho kimekuwa kikifanya msako dhidi ya mawakili bandia nchini kupitia kwa timu yake ya kuchukua hatua kwa kasi maarufu kama Rapid Action Team, RAT.
Hata hivyo, muungano wa COTU kupitia Katibu Mkuu wake Francis Atwoli unatofauatiana na msimamo wa LSK kuhusiana na “wakili” Njagi.
Katika taarifa, COTU ilimtetea Njagi ikisema inaamini mno katika kanuni ya kutambuliwa kwa mafunzo ya awali, yaani Recognition of Prior Learning (RPL), ambayo yanatambua na kuthamini uelewa, ujuzi na umilisi ambao mtu ameupata kupitia njia zisizokuwa za kawaida za mafunzo.
“Kisa cha Brian Njagi kinaibua maswali ya msingi kuhusiana na upatikanaji na ujumuishaji wa taaluma nchini Kenya. Ikiwa ni kweli kwamba Brian amehudumu kama wakili na kufanikiwa kuwawakilisha wateja wake kuhusiana na masuala ya sheria, tunatoa wito wa dhati kwamba tathmini ifanywe kwa usawa na uwazi kubaini uelewa wake, ujuzi na umilisi katika nyanja ya sheria,” alisema Atwoli katika taarifa leo Ijumaa.
Anasema COTU inatambua kuwa Kenya ni ngome ya vijana walio na ujuzi wa hali ya juu na wenye vipaji tele ambao wamepata ujuzi wao kupitia tajriba ya kivitendo, kujisomea na njia zisizokuwa rasmi za elimu.
“Watu hawa, licha ya uwezo wao maridhawa, mara nyingi hujipata wakinyimwa nafasi za kazi katika sekta rasmi kwa sababu mfumo kwa kawaida hutoa kipaumbele kwa watu waliofuzu kupitia njia za kawaida za mafunzo,” aliongeza Atwoli.