Home Burudani Wakfu wa Profesa Jay wazinduliwa

Wakfu wa Profesa Jay wazinduliwa

0

Mwanamuziki na mwanasiasa wa Tanzania Profesa Jay hatimaye amezindua wakfu wake ambao unalenga kusaidia wanaougua maradhi ya figo.

Uzinduzi huo ulifanyika jana jioni katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam na ulihudhuriwa na watu kadhaa wakiwemo wendani wake kisiasa na viongozi wa serikali.

Naibu waziri wa Afya Daktari Godwin Mollel ndiye aliongoza uzinduzi wa wakfu huo kwa niaba ya Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa.

Bi. Anna Tibaijuka ambaye ni mmoja wa washauri wakuu wa wakfu wa Profesa Jay naye alikuwepo.

Makamu mwenyekiti wa chama cha CHADEMA ambapo Jay ni mwanachama Tundu Lissu alihudhuria uzinduzi huo na kuchangia shilingi milioni 2 pesa za Tanzania.

Lissu alimpa pole Profesa Jay kwa kuugua akisema kwamba hakuweza kumtembelea akiwa hospitali lakini akakumbuka jinsi Jay alimzuru hospitalini Nairobi wakati alikuwa amelazwa.

Mwanamuziki Lady Jaydee aliahidi milioni 5, Kings Music ya Ali Kiba milioni 5, Weusi Milioni 1, Chege na Temba wakaahidi milioni 1 na timu ya soka ya Yanga milioni 5.

Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi kuchangia milioni 50 kwa wakfu huo ingawa hakuhudhuria uzinduzi binafsi.

Alipozungumza, Profesa Jay alishukuru wote ambao wamesimama naye kwenye safari ya maandalizi ya uzinduzi wa wakfu huo akisema utahusisha wote bila kuzingatia miegemeo ya kisiasa wala dini.

Website | + posts